Click here to view Mama Ye! Tanzania in English

Mwanzo > Kuhusu Mama Ye!

Kuhusu Mama Ye!

Dhamira yetu

Mama Ye! ni kampeni inayohusu kufanya mabadiliko ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga wa Tanzania. Mama zetu na watoto wachanga wengi mno wanaendelea kufa wakati wa ujauzito na kujifungua – la kusikitisha ni kwamba vifo hivyo vingi vinazuilika! Kwa kubadilisha mtazamo wa kukata tamaa uwe wa matumaini; dhana ya kutoweza jambo iwe ya kuchukua hatua; Masuala  ya uhai wa mama yasiachwe kando ila yapewe kipaumbele cha kisiasa; na ukisiaji jinsi hali halisi ilivyo uachwe ila utafutwe uhakika uliopo. Mama Ye! inawakilisha harakati za umma kutetea uhai wa mama zetu na watoto wetu wachanga.

Tunajua mabadiliko yanawezekana kwa sababu kila siku, wanaume na wanawake wa Tanzania kama wewe huchukua hatua ya kufanya mabadiliko, na huokoa maisha. Madereva wa teksi ambao hupeleka wanawake wajawazito kliniki usiku wa manane; viongozi wa serikali za mitaa ambao hufanya vifaa vya tiba vipatikane kwa wingi na kirahisi; wanafunzi ambao huchangia damu; waandishi wa habari ambao huliweka suala hili hai; wanasiasa ambao huipa kipaumbele afya ya mama; vikundi vya jamii ambavyo hufuatilia ahadi za wanasiasa; na wanawake vijana wanaochukua mafunzo ya kuwa wakunga, ambao watajitolea maisha yao kuwatunza kina mama na watoto.

Mama Ye! inawashangilia na kutambua mchango wa mashujaa hao mmoja mmoja na pia mashirika nchini kote Tanzania ambao hufanya kazi bila kuchoka na kufanya ujauzito na uzazi kuwa salama, ili wengine waweze kutiwa moyo na kuhamasishwa kufanya hivyo pia.

Mama Ye! hukuwezesha kupata taarifa na ushahidi ili uhoji, uchambue, ulinganishe, uelewe, utetee na kuchukua hatua kwa ajili ya mabadiliko chanya.

Sio tu kuelewa ushahidi ulio katika lugha ya kitaalaamu bali hata kutafuta kituo kilicho karibu nawe ambapo unaweza kuchangia damu kwa hiari; kufahamu miongozo mipya zaidi ya kitabibu, hadi ufuatiliaji wa kuishiwa bajeti au madawa; Mama Ye! huweka habari mikononi mwa wale walio na utashi wa kufanya mabadiliko. Kupitia mapinduzi ya mawasiliano ya simu za mkononi Tanzania, Mama Ye! inakuunganisha wewe na wengine walio na lengo kama lako.

Mama Ye! ni kampeni kwa ajili yetu sote, na ifanywayo nasi sote, ili kuhakikisha kina mama na watoto wachanga Tanzania wananusurika katika kipindi cha ujauzito na kujifungua. Sisi sote kwa pamoja ni Mama Ye!

 

Evidence for Action

Mama Ye! ni kampeni iliyoanzishwa na Evidence for Action, (ikimaanisha Ushahidi kwa Utekelezaji) mpango wa miaka kadhaa ambao unakusudia kuboresha maisha ya kina mama na watoto wachanga katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mpango huu unaofadhiliwa na Idara ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), unalenga kutumia mikakati mchanganyiko ya ushahidi, utetezi, na uwajibikaji ili kuokoa maisha nchini Ghana, Malawi, Nigeria, Ethiopia, Sierra Leone na Tanzania.